RAIS DKT. MWINYI AHIMIZA MALEZI BORA NA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa jamii kuunganisha nguvu katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa kuimarisha malezi bora ya watoto na vijana, ili kulinda nguvu kazi na mustakabali wa Taifa.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo, tarehe 26 Juni 2026, aliposhiriki Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al Azhar, Mpendae, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema malezi bora yanayoanzia ndani ya familia na kuzingatia mafunzo ya dini ndiyo msingi wa kujenga vijana wenye maadili na kuwakinga dhidi ya dawa za kulevya, uhalifu na vitendo vingine viovu.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi Mabaya na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya yatakayofanyika tarehe 27 Juni yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika kutokomeza tatizo hilo.
Katika kuadhimisha siku ya Ashura, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza waumini kuongeza ibada, kufunga, kutenda mema na kuendelea kuwalea watoto na vijana katika misingi ya maadili, uadilifu, huruma na kumcha Mwenyezi Mungu.



