TUME YA TAIFA UMWAGILIAJI YAKUTANA KUBORESHA USIMAMIZI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI (NIRC)
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewakutanisha Menejimenti, wahandisi wa Mikoa. Wakandarasi na washauri elekezi kujadili namna ya kuboresha usimamizi wa miradi ya umwagiliaji (NIRC)
Kikao hicho kilifanyika Mjini Dodoma ambapo kimewakutanisha viongozi hao akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, Menejimenti ya Tume,Wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa, wakandarasi na washauri elekezi wanaotekeleza miradi ya Umwagiliaji nchini, kwa lengo la kujadili utaratibu mpya wa usimamizi wa miradi ya Umwagiliaji, ili kuwa na matokeo bora na kwa wakati.
Katika kikao hicho, washiriki wamejadili kwa kina hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi inayoendelea na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Aidha, wamejadili mgawanyo wa majukumu na namna bora ya kushirikiana katika kusimamia miradi kupitia mfumo wa usimamizi wa miradi ya Umwagiliaji kupitia washauri elekezi (Consultants)
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa amewataka wahandisi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa washauri elekezi kusimamia, kulinda na kutunza kikamilifu mali za umma .
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu, wa Tume, Leopold Runji, amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya taarifa sahihi na kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu ili kufanikisha malengo ya Serikali katika sekta ya Umwagiliaji.
Washauri elekezi walioshiriki kikao hicho wameipongeza Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kuwaamini na kuwapa jukumu la kusimamia miradi, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji..



