SERIKALI KUKABILIANA NA MATUKIO YA DHARURA NA MAJANGA NDANI NA NJE YA NCHI



Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Dharura na Maafa inaendelea kutekeleza afua za Kuimarisha utayari na uwezo wa kukabiliana na Majanga na dharura zingine za afya ya jamii ikiwemo kutuma timu za haraka za kukabiliana na matukio ya Dharura hizo (Deployment of Rapid Response Team) kwa lengo la kukabiliana na matukio ya dharura ndani na nje ya nchi.


Hayo yamesemwa Leo  tarehe 4 Juni, 2026 Mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Kitengo cha  Dharura na Maafa Wizara ya Afya  Dkt. Erasto Sylvanus wakati akifungua kikao kazi cha timu ya Wataalam kutoka Wizara mtambuka kwa dhana ya Afya moja kushiriki zoezi la "table-top simulations exercise" ili kupima kwa vitendo matumizi ya Mwongozo wa Kutuma Timu ya Wataalam kukabiliana na dharura ndani na nje ya nchi (Personnel Deployment Guideline).


Amesema kuwa, Tanzania kupitia Wizara ya Afya Kitengo cha Dharura na Maafa  imeendelea kujiimarisha na kujipanga vema kwa kuwaandaa Wataalam wa Afya  kuweza kukabiliana na Majanga na dharura zinazoweza kujitokeza kama vile Ebola, Marburg na dharura zingine zenye athari kwa Afya ya jamii.


"Napenda kuwahakikishia Wananchi na jamii ya Watanzania kuwa Serikali yetu imejizatiti kuchukua tahadhari katika maeneo yote ikiwemo mipakani mwa Nchi zilizokumbwa na  ugonjwa  wa Ebola kama Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na katika jamii kwa ujumla. Wataalam wa Afya wamejipanga na elimu mbalimbali inaendelea kutolewa kwa Wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari ili ugonjwa usiingie nchini", amesema Dkt.Erasto Sylvanus


Aidha, Dkt.Erasto amewashukuru Wataalam wa Afya hapa nchini kwa jinsi wanavyoendeleea kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa Wananchi wakati wa Dharura na Majanga na kuwataka wataalam hao kuwa tayari kuwasaidia wenzetu wa Nchi zingine zilizoathirika wakati huu wanapopita katika hatari ya ugonjwa wa Ebola kutokana na uwezo mkubwa wa wataalam wetu na mafunzo mbalimbali waliyopata.


"Hadi sasa Tanzania bado ipo salama kwani hakuna mgonjwa aliyethibitika nchini na tujitahidi ibaki hivyo. Naomba kusisitiza kuwa Wananchi na jamii tuendelee kuchukua tahadhari zaidi kwa kufuata maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Wataalam wa Afya na Viongozi wetu wa Serikali" amesema Dkt.Erasto Sylvanus.


Naye Dkt.Faraja Msemwa Afisa wa Utayari wa kukabiliana na Dharura na Majanga kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO),ametoa Pongezi kwa Tanzania kupitia Wizara ya Afya  kwa kuwa mfano bora miongoni mwa Nchi za Afrika kwa kuandaa kwa haraka Mwongozo utakaowasaidia Timu ya Wataalam kupelekwa maeneo mbalimbali ili kupambana na Dharura ndani na nje ya Nchi.


"Shirika la Afya Duniani linajivunia hatua mathubuti iliyochukukiwa na Tanzania ya kuandaa Mwongozo huu ambao sina  uhakika kama Nchi nyingi za Afrika zinazo kwa sasa, Tanzania imeonesha Utayari na ushirikiano wa dhati katika kufuata Kanuni za Afya Kimataifa "International Health Regulations". WHO inaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na dharura mbalimbali" amesema Dkt.Msemwa.


Kwa upande wake Bi.Mwanaisha Mrisho kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu Sera na Bunge ameipongeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani kwa jinsi ilivyosimamia kuanzisha na kupatikana kwa Mwongozo huu. Kupatikana kwa Mwongozo ni hatua muhimu ya Tanzania katika kusimamia vema pamoja na kuimarisha  masuala ya Afya nchini kwa kuzingatia viwango vya  Kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani(WHO).

Powered by Blogger.