TASNIA YA SANAA YAPATA PIGO LINGINE MSANII MKONGWE MZEE ONYANGO AFARIKI DUNIA
Tasnia ya sanaa ya maigizo nchini Tanzania imegubikwa na simanzi kufuatia taarifa za kifo cha muigizaji Mkongwe Issa Joseph maarufu Mzee Onyango.
Mzee Onyango alikuwa miongoni mwa wasanii waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa maigizo ya Tanzania kupitia vipaji vyake vya uigizaji, vichekesho na uwezo wa kuwasilisha ujumbe kwa njia iliyowagusa watazamaji wa rika mbalimbali.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa asubuhi ya leo na Msanii mwenzie Seif Mbembe ambaye amesema Marehemu Onyango aliyejizolea heshima kubwa kutokana na umahiri wake wa kuigiza wahusika waliobeba mafunzo, burudani na taswira halisi ya maisha ya jamii, amefariki dunia leo alfajiri.
Kwa miaka mingi, jina lake limeendelea kubaki kwenye kumbukumbu za mashabiki wa filamu na maigizo ya Kitanzania. Wengi watamkumbuka kwa uchangamfu wake, uhalisia wa uigizaji wake na mchango wake katika kuwalea na kuwahamasisha wasanii chipukizi.
Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu pamoja na jamii nzima ya wasanii.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Wasanii hufariki, lakini kazi zao huendelea kuishi katika mioyo ya watu.

