TMDA YAIHAKIKISHIA KAMATI YA BUNGE UDHIBITI WA DAWA FEKI NA DUNI NCHINI

 




Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI juu ya kuendelea kuimarisha udhibiti wa dawa feki na duni nchini kwa lengo la kulinda afya za wananchi na kuboresha utoaji wa huduma za afya.


Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati wa ziara ya mafunzo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI iliyofanyika leo Juni 10, 2026, kwa lengo la kujifunza huduma zinazotolewa na TMDA chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya.


Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuwekeza vya kutosha katika rasilimali mbalimbali ikiwemo vifaa vya kisasa, mifumo ya uchunguzi pamoja na wataalamu ili kubaini dawa duni na feki kabla hazijaleta madhara kwa wananchi.


Amesema uwekezaji huo umeiwezesha TMDA kuimarisha uwezo wa udhibiti wa ubora wa dawa na vifaa tiba vinavyoingia na vinavyotumika nchini, hatua inayosaidia kuhakikisha wananchi wanapata dawa salama, bora na zenye ufanisi.


“Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha afya na usalama wa Watanzania vinaendelea kulindwa,” amesema Dkt. Samizi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, ameipongeza TMDA kwa kazi kubwa ya kusimamia ubora wa dawa na vifaa tiba nchini.


Aidha, ameishauri Serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika rasilimali mbalimbali zitakazowezesha kubaini kwa ufanisi dawa duni na feki pamoja na vifaa tiba visivyo salama, ili kuimarisha ulinzi wa afya za Watanzania.


Amesema jitihada hizo zitasaidia kuongeza imani ya wananchi katika mfumo wa afya na kuhakikisha bidhaa za afya zinazotumika nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Powered by Blogger.