WAKAGUZI WA CAF WARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MABORESHO YA VIWANJA VYA AFCON 2027





Wakaguzi kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Bw. Lakshmikanth Karunanithi na Bw. Eduard Captan, wamefanya ukaguzi wa miundombinu ya viwanja vinavyotarajiwa kutumika katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), na kueleza kuridhishwa na hatua ya maboresho yanayoendelea.

Katika ziara hiyo, wakaguzi hao walitembelea Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo walikagua maendeleo ya maboresho ya sehemu ya kuchezea (pitch), maeneo maalumu ya wageni na viongozi mashuhuri (VVIP), pamoja na sehemu zitakazotumika na wanahabari wakati wa mashindano.

Mbali na Uwanja wa Benjamin Mkapa, ujumbe huo pia ulitembelea viwanja vya mazoezi vya Gymkhana II na Faras, ambavyo vinajiandaliwa kuhudumia timu zitakazoshiriki AFCON 2027.




Baada ya ukaguzi huo, wakaguzi wa CAF walieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa maboresho pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, wakibainisha kuwa hatua zilizofikiwa zinaonyesha dhamira ya kuhakikisha viwanja vinakidhi viwango vinavyohitajika kwa ajili ya mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.

Ukaguzi huo ni sehemu ya tathmini ya mara kwa mara inayofanywa na CAF ili kufuatilia maandalizi ya nchi mwenyeji kuelekea AFCON 2027, kuhakikisha miundombinu yote inakamilika kwa ubora na kwa wakati.
Powered by Blogger.