CCM YAPONGEZA MABORESHO HUDUMA ZA AFYA IGUNGA
Na Mwandishiwetu, Igunga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kufurahishwa na maboresho makubwa ya huduma za afya yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora na maeneo mengine.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Komredi Said Nkumba alipokuwa akiongea na wakazi wa Wilaya hiyo kwenye ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa iliyotembelea Wilaya hiyo jana kukagua utekelezaji ilani.
Ameeleza kuwa maboresho hayo ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa pia.
‘Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi ili kuharakisha utekelezaji miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji huduma kwa jamii, pia naipongeza halmashauri hii kwa kutenga fedha za ndani ili kukamilisha mradi huu’, ameeleza.
Komredi Nkumba ameagiza Viongozi na Wataalamu wa halmashauri hiyo kusimamia ipasavyo miundombinu na huduma zinazotolewa ili ziwe endelevu na kunufaisha wananchi wote.
Aidha amepongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi na kuwajengea daraja la kudumu la mawe linalounganisha kata 2 za Nyandekwa na Ntobo Kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Mwanne Mchemba ameeleza kufurahishwa na maboresho ya huduma katika Hospitali hiyo.
‘Wajumbe wote tumeridhishwa na kazi iliyofanyika katika Hospitali hii na mradi wa daraja, hakika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imetekelezwa kwa vitendo’, ameongeza.
Awali akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Naitwapak Tukai amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo kuboresha miundombinu ya huduma za afya.
Amebainisha kuwa kazi yao ni moja tu kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa na serikali katika Wilaya zote za Mkoa huo ili ikamilike kwa wakati na kulinda miundombonu ya yake..




