DC MAPUNDA:TAMAA YA MAISHA YA HARAKA YAWAINGIZA VIJANA KWENYE DAWA ZA KULEVYA






Na Mwandishi wetu--Dar es salaam 


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema sababu kubwa inayowasukuma baadhi ya vijana kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya ni tamaa ya kuishi maisha ya kifahari yasiyolingana na kipato chao, baada ya kuvutiwa na maisha ya baadhi ya wenzao.

Mapunda ameitoa kauli hiyo Julai 23, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa tamasha la "Kataa Dawa za Kulevya, Timiza Malengo Yako", lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA). Alisema tamasha hilo linalenga kushirikisha wananchi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kama sehemu ya mkakati wa mwaka 2026 wa kuimarisha vita hivyo katika ukanda wa mashariki mwa Tanzania.

"Niwatake vijana tukatae dawa za kulevya kwa moyo mmoja. Suala hili ni gumu sana kwa sababu tunapoteza nguvu kazi ya Taifa. Madhara ya dawa za kulevya hayaji kwa siku moja, bali humuangamiza mtumiaji taratibu na mwisho wake huwa ni mabaya sana," alisema Mapunda.

Aidha, alieleza kufurahishwa kwake kuona tamasha hilo linafanyika Wilaya ya Temeke, akisema eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika na tatizo la dawa za kulevya. Alitaja maeneo ya Buza na Magurumbasi kuwa na baadhi ya watu wanaodaiwa kutumia biashara za uuzaji wa magari kama mwamvuli wa shughuli za usambazaji wa dawa hizo.




Mapunda amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina katika baadhi ya showroom za magari zilizopo Temeke ili kubaini iwapo zinatumika kutakatisha fedha zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya.

"Haiwezekani mtu atoke mkoani na kusema amekuja Buza au Magurumbasi kununua gari. Vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa shughuli hizo," amesisitiza.
Aliongeza kuwa njia mojawapo ya kutokomeza tatizo la dawa za kulevya ni kuvunja mnyororo wa usambazaji wake pamoja na kupunguza idadi ya watumiaji kupitia utoaji wa elimu kwa watoto, vijana na wazazi kuhusu madhara ya dawa hizo.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Kinga na Tiba wa DCEA, Dk. Cassian Nyandindi, alisema takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2022 zaidi ya watu 14,000 wamepata huduma za matibabu katika Kitengo cha Afya ya Akili cha Hospitali ya Temeke kutokana na uraibu wa dawa za kulevya.



Dk. Nyandindi ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana na DCEA kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu wahusika wa biashara haramu ya dawa za kulevya kupitia namba 119, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni silaha muhimu katika kuilinda jamii dhidi ya athari za dawa hizo.


Powered by Blogger.