JESHI LA POLISI LAMKAMATA "MAOPENA" KWA TUHUMA ZA KUWAUA BABA YAKE NA BABA YAKE MDOGO

 



Na Mwandishi wetu-Dar es salaam


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata Hosamu Hamza Juma, maarufu kwa jina la Maopena, kwa tuhuma za kuwaua baba yake mzazi, Hamza Juma Omari (48), na baba yake mdogo, Ally Juma Omari (37), kisha kufukia miili yao kwenye shimo lililokuwa katika eneo la nyumba yao, Mtaa wa Sindano, Mwananyamala.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Faustine Mafwele, amesema uchunguzi ulianza baada ya Hamza Juma Omari kuripotiwa kutoweka katika Kituo cha Polisi Oysterbay. Alisema wakati mahojiano na uchunguzi ukiendelea, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa wananchi zikieleza kuwapo kwa damu nyingi katika nyumba ya familia hiyo.


SACP Mafwele amesema uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na Jeshi la Polisi ulibaini kuwa watu hao wawili walikuwa wameuawa na miili yao kufukiwa kwenye shimo ndani ya eneo la makazi hayo. Kufuatia uchunguzi huo, mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, 2026, eneo la Makongo majira ya saa 9:00 alasiri akiwa na kisu kinachodaiwa kutumika kutekeleza uhalifu huo pamoja na mavazi yaliyokuwa yamechafuliwa damu.


Jeshi la Polisi limesema chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika na kinaendelea kufanyiwa uchunguzi. Aidha, limetoa shukrani kwa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wao uliowezesha kubainika kwa tukio hilo, huku likisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa endapo atabainika kuhusika.

Powered by Blogger.