MUHIMBILI, MEGA WE CARE WATOA HUDUMA BURE ZA UCHUNGUZI NA CHANJO YA HOMA YA INI
Na Mwandishi wetu-Dar es salaam
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa kushirikiana na kampuni ya Mega We Care Tanzania Limited, imeanza kutoa huduma za uchunguzi, chanjo na ushauri kuhusu ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis) bure kwa wananchi kwa muda wa siku mbili.
Kambi hiyo ya huduma za afya imeanza Julai 28 na itaendelea hadi Julai 29, 2026, katika IDC Clinic, iliyopo karibu na Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR) katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi ambao kutokana na majukumu yao ya kila siku hukosa muda wa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na kinga dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ini kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Swaleh Kitabu Pazi, amesema idadi ya wagonjwa wa homa ya ini wanaohudumiwa katika hospitali hiyo imeendelea kuongezeka, hali inayosisitiza umuhimu wa kuongeza huduma za uchunguzi na kinga kwa jamii.
Dkt. Pazi amesema kliniki ya homa ya ini ya Muhimbili kwa sasa inahudumia takribani wagonjwa 5,000 waliosajiliwa, huku wastani wa wagonjwa 100 wakifika kliniki hiyo kila siku kwa ajili ya matibabu na ufuatiliaji wa afya zao.
Ameeleza kuwa njia kuu za maambukizi ya virusi vya homa ya ini aina ya B ni pamoja na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au wakati wa kujifungua, kujamiiana bila kinga, kuongezewa damu isiyo salama pamoja na kutumia kwa pamoja vifaa vyenye ncha kali kama vile sindano.
Aidha, Dkt. Pazi amesisitiza kuwa virusi vya homa ya ini haviambukizwi kwa njia ya mate wala jasho, huku akiwataka wananchi kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumzia hali ya homa ya ini duniani, Dkt. Pazi amesema zaidi ya watu milioni 500 wanaishi na virusi vya homa ya ini, huku takribani watu milioni 1.3 wakifariki dunia mwaka 2024 kutokana na madhara yanayohusishwa na virusi vya homa ya ini aina ya B na C.
Amesema changamoto kubwa ni kuwa wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, jambo linalopunguza uwezekano wa kupata matokeo mazuri ya matibabu.
Kwa sababu hiyo, amewahimiza wananchi kujitokeza kupima afya zao mapema na kupata chanjo, akieleza kuwa homa ya ini aina ya B inaweza kuzuilika kwa chanjo, huku homa ya ini aina ya C ikiwa na tiba inayoweza kuponya
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Mega We Care Tanzania Limited, Mengi Ntasimba, amesema kampuni hiyo imeungana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuandaa kambi hiyo ikiwa ni sehemu ya kurejesha mchango kwa jamii baada ya kampuni hiyo kuhudumu nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 20.
Amesema Mega We Care imechangia vifaa vya uchunguzi pamoja na dawa kwa wagonjwa watakaobainika kuwa na maambukizi, huku ikiendelea kutekeleza programu mbalimbali za elimu ya afya katika jamii na taasisi za elimu.
Naye mmoja wa wananchi waliojitokeza katika kambi hiyo, Joseph Daniel Chengula, mkazi wa Kimara Mwisho na mfanyabiashara wa Kariakoo, amesema alipata taarifa kuhusu huduma hiyo kupitia mitandao ya kijamii na kuamua kufika mapema kwa ajili ya kupima na kupata chanjo.
Chengula amesema huduma hiyo ni muhimu kwake kwa kuwa inampa uhakika wa afya yake hata anaposafiri kwenda nje ya nchi.
Huduma hizo zinaendelea kutolewa katika kambi hiyo, huku wananchi wakihimizwa kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi na kupata uchunguzi, ushauri pamoja na chanjo ya homa ya ini bila malipo.




