WALIMU SIKONGE WAPEWA ELIMU YA MALEZI BORA





 Na mwandishi wetu, Tabora

WALIMU Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kulea wanafunzi katika maadili yanayofaa ili watakapomaliza masomo wawe na tabia njema miongoni mwa jamii.

Aidha wametakiwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa na serikali katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za elimu kwa watoto wawapo shuleni.



Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Selemani Pandawe alipokuwa akifungua mafunzo ya malezi na unasihi kwa walimu na wanafunzi yanayoratibiwa na Shirika la UNICEF Wilayani hapa.

Pandawe amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kubahatisha, bali wazingatie taratibu, sheria na miongozo inayotolewa na Wizara ya Elimu ili wanafunzi walelewe katika njia zinazofaa.

‘Mwalimu unapopata jambo lolote mezani kwako huna haja ya kutafuta ufumbuzi mwenyewe, serikali imeshatoa maelekezo na miongozo katika kila eneo, ukiifuata, utafanya maamuzi sahihi na kutekeleza wajibu wako kwa ufanisi,’ ameeleza.

Pandawe amebainisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana hivyo akawataka Wakuu wa Shule kuwapunguzia vipindi walimu wa malezi na unasihi ili wawe na muda wa kutekeleza jukumu hili la malezi pia.

‘Hili ni jukumu muhimu sana shuleni, Wakuu wa shule msiwarundikie vipindi vingi hawa walimu, wakikosa muda wa kutosha wanafunzi watakosa huduma hii muhimu ambayo huchochea ustawi wao wa kitaaluma na kijamii’, ameongeza.



Mwezeshaji wa mafunzo hayo na Mwakilishi wa UNICEF, Buheri Thomas, amefafanua kuwa mafunzo hayo ya siku mbili ymealenga kuwajengea uwezo walimu wa malezi na unasihi ili waweze kujenga kizazi chenye maadili.



Mkuu wa Shule ya Sekondari Pangale, Sengi Bahiu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mafunzo hayo amewataka walimu kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kurekebisha tabia za wanafunzi.

 Mwisho
Powered by Blogger.