UYUI YAANZISHA MIRADI KUCHOCHEA KASI YA MAENDELEO
Na Mwandishi wetu, Tabora
HALMASHAURI ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora imedhamiria kuongeza mapato zaidi kupitia vyanzo vyake vya ndani kwa kuanzisha miradi ya kimkakati ili kuchochea kasi ya maendeleo ya wananchi.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Shaban Katalambula ambaye ni diwani wa Kata ya Goweko alipokuwa akitoa taarifa ya miradi ya halmashauri kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.
Amesema kuwa licha ya kuwa na vyanzo kadhaa vya mapato halmashauri imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa vibanda vya biashara katika eneo la stendi ya mabasi ambavyo vitakavyokodishwa kwa wananchi.
‘Mradi huu utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 74 unatarajia kuongeza mapato ya halmashauri kwa kiasi kikubwa hivyo kuchochea kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi’, ameeleza.
Amedokeza kuwa halmashauri imeendelea kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kupata mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mzuri wa Ofisi ya Mkurugenzi, Wataalamu, Watendaji, Madiwani na Chama tawala (CCM).
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Uyui Said Lubasha Makoba amepongeza mikakati mizuri ya halmashauri hiyo kwa kuwa itasaidia kupanua wigo wa utekelezaji miradi ya maendeleo ikiwemo kutatua kero za wananchi.
Mbunge Mstaafu na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa Lucas Selelii amekiri kuwa licha ya halmashauri hiyo kuwa changa, kasi yake ya maendeleo ni kubwa, hivyo akawataka kuongeza ubunifu na mshikamano ili kufanikisha mipango yao.
Akitoa salamu za Chama kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Nassoro Hamdan amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Uongozi wa Halmashauri na Kamati ya Siasa ya Wilaya.
Amewataka kusimamia ipasavyo utekelezaji miradi yote katika Wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya CCM Wilaya ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na hatimaye kupiga hatua kubwa kimaendeleo.



