KURASINI LOJISTIKI PARK KUONGEZA UWEZO WA BANDARI YA DAR ES SALAAM – PROF. MBARAWA*
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, leo tarehe 21 Agosti,2026 ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kurasini Lojistiki Park, jijini Dar es Salaam, linalojengwa kwa ajili ya kutumika kama Bandari Kavu (Dry Port) na baadaye kuwa sehemu ya miundombinu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
Prof. Mbarawa amesema Kurasini Lojistiki Park inatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Novemba mwaka huu, ikiwa ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza msongamano wa mizigo katika eneo kuu la bandari
Amesema eneo hilo linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia hadi makasha 700,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na uwezo wa sasa wa Bandari ya Dar es Salaam wa takribani makasha 344,000 kwa mwaka, hivyo kuongeza ufanisi wa kuhudumia shehena zinazopita bandarini
Mbarawa amesema Kurasini Lojistiki Park itatumika kwa shughuli za uhifadhi, ukaguzi, clearance na usambazaji wa mizigo, huku sehemu ya shughuli hizo ikihamishiwa katika eneo hilo ili kupunguza presha katika Bandari ya Dar es Salaam
Aidha, amesema eneo hilo litakuwa na maegesho maalumu ya malori, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa malori katika barabara zinazozunguka bandari na kuboresha mtiririko wa magari yanayohudumia shughuli za usafirishaji wa mizigo
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Bw. Abed Gallus, amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa mizigo na malori, pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli za ukaguzi, clearance na utoaji wa mizigo
Kurasini Lojistiki Park inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuongeza uwezo na ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam, kuboresha huduma kwa wafanyabiashara na watumiaji wa bandari, na hatimaye kuimarisha ufanisi wa usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.


