NEEMA YAWASHUKIA WAKULIMA WA TUMBAKU
Na Mwandishiwetu, Tabora
BODI ya Tumbaku (TTB) imetangaza kuwa bei ya tumbaku msimu ujao wa kilimo itakuwa Dola za Kimarekani 2.5 kwa kilo sawa na shilingi 6,000 au zaidi kutokana na kiwango cha kubadilishia fedha (exchange rate) cha wakati huo.
Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugenzi wa Bodi hiyo Stanley Nozya alipokuwa akiongea na Wataalamu, Wakuu wa Taasisi, Madiwani, Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya Mkoa.
Ameeleza kuwa katika msimu uliopita wakulima hawakufurahishwa na bei ya soko ambayo ilikuwa Dola za Kimarekani 1.92 sawa na shilingi 4,800 hadi 4,900 kwa kilo hali iliyoibua malalamiko mengi na wengine kugoma kuuza tumbaku yao.
‘Zao hili limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi kwenye soko la dunia, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, lakini serikali imeendelea kufanya juhudi kubwa, ili kuhakikisha zao hili linakuwa na tija kubwa kwa mkulima’, ameongeza.
Baada ya juhudi hizo, habari njema ni hii, katika msimu ujao wa kilimo mkulima atauza kilo moja ya tumbaku kwa Dola za Kimarekani 2.5, hii ni neema kwa wakulima kwani itawachochea kuongeza uzalishaji zaidi na kulima kwa tija pia.
Nozya amebainisha kuwa bei nzuri ya zao hilo huamliwa kwa ubora wake, lakini akakiri kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa hawazingatii kanuni za kilimo bora hali inayopelekea kuzalishwa tumbaku isiyo na ubora na yenye uchafu.
‘Changamoto za wakulima tutazitatua kwa pamoja, tutaandaa semina kwa ajili ya viongozi, wadau na wakulima ili kuwapa uelewa wa zao hili na mwenendo mzima wa soko la dunia na kupokea maoni na ushauri wao,’ tutawajulisha siku’, ameeleza.
Amedokeza kuwa mwafaka wa bei mpya ya msimu ujao umefikiwa baada ya majadiliano ya kina na makampuni wanunuzi, hivyo akashauri wakulima kuandaa mashamba yao mapema na kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Aidha aliongeza kuwa suala la mbolea halina mjadala, Waziri wa Kilimo ameshaagiza mbolea ifike kwa wakulima mapema iwezekanavyo na wasambazaji wajulikane mapema na wasimamiwe ipasavyo, na hili litalizingatiwa.
Pia amedokeza kuwa wamepata wanunuzi wapya wawili wakubwa ambao wataanza kununua zao hilo kuanzia msimu ujao, makampuni hayo yatatangazwa muda si mrefu.


