MFUMO WA T-CAMS MAGEUZI YA KIDIJITALI KULETA UFANISI SEKTA YA UWAKALA WA FORODHA TANZANIA

 





Utangulizi


Katika dunia ya sasa, ushindani wa biashara haupimwi tena kwa ukubwa wa bandari au idadi ya mipaka ya nchi, bali kwa ubora wa mifumo inayorahisisha biashara. Mataifa mengi yanayofanikiwa katika biashara ya kimataifa yamewekeza katika mifumo ya kidijitali inayopunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuhakikisha kila mdau anapata haki yake kwa wakati.


Tanzania imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji na biashara kupitia uwekezaji katika Bandari, Reli ya Kisasa (SGR), viwanja vya ndege, barabara na mifumo ya ukusanyaji wa mapato. Ili uwekezaji huo utoe matokeo yaliyokusudiwa, ni muhimu kuwe na mifumo ya kisasa inayosimamia huduma za uwakala wa forodha.



Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) wamekuja na Mfumo wa Tanzania Customs Agent Management System (T-CAMS) uliotengenezwa na kampuni ya Capital Pay Ltd iliyosajiliwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya mageuzi hayo. 



Mfumo huu unaoshirikisha TRA unalenga kuleta uwazi katika malipo, kulinda heshima na maslahi ya mawakala wa forodha, kurahisisha huduma kwa waagizaji wa mizigo na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mfumo huu pia ni utekelezaji wa tangazo katika gazeti la serikali (GN) namba 83 la Machi, 2026 lililotolewa na shirika la uwakala wa meli Tanzania (TASAC). 


Changamoto Zilizokuwepo


Kwa miaka mingi, sekta ya uwakala wa forodha ilikabiliwa na changamoto kadhaa.

Kwanza, kulikuwa na migogoro ya malipo kati ya mawakala na waagizaji wa mizigo. Mara nyingi wakala alikamilisha kazi lakini malipo yalicheleweshwa au hayakulipwa kabisa.


Pili, kulikuwepo ushindani usio wa haki ambapo baadhi ya mawakala walishusha gharama za huduma kwa kiwango kisichoendana na ubora wa kazi ili kupata wateja.


Tatu, mfumo usio rasmi wa malipo uliifanya Serikali kushindwa kupata taswira sahihi ya mapato yanayotokana na sekta hii, jambo lililofungua mianya ya ukwepaji wa kodi na kupunguza uwazi.


T-CAMS ni Nini?


T-CAMS ni mfumo wa kidijitali unaounganisha malipo ya kodi za forodha na ada ya wakala katika utaratibu mmoja ulio wazi na unaofuatilika.


Kupitia mfumo huu, mteja analipa kwa utaratibu rasmi, ambapo kodi za Serikali na ada ya wakala zinashughulikiwa kwa uwazi. Hii inapunguza migogoro ya malipo na kuongeza uaminifu katika mnyororo mzima wa biashara.


Faida kwa Mawakala wa Forodha


Mfumo huu unaleta mabadiliko makubwa kwa mawakala wa forodha.


Kwanza, unahakikisha wakala analipwa kwa wakati, hivyo kupunguza madeni na migogoro iliyokuwa ikiathiri biashara zao.


Pili, unajenga mazingira ya ushindani wa haki. Badala ya kushindana kwa kushusha bei kupita kiasi, mawakala watashindana kwa ubora wa huduma, utaalamu na matumizi ya teknolojia.


Tatu, historia ya mapato inayopatikana kupitia mfumo inaweza kuongeza uwezo wa mawakala kupata mikopo, kuvutia wawekezaji na kupanua biashara zao.


Nne, taaluma ya uwakala wa forodha inapata hadhi zaidi kwa kuwa huduma zake zinasimamiwa kupitia mfumo rasmi unaotambulika.


Faida kwa Waagizaji wa Mizigo


Waagizaji wa mizigo watanufaika kwa kupata mfumo wenye uwazi na unaotabirika.


Watakuwa na uelewa wa gharama wanazopaswa kulipa kabla ya huduma kukamilika, jambo litakalowasaidia kupanga bajeti na kupunguza migogoro.


Aidha, kwa kuwa malipo ya wakala yanahakikishwa kupitia mfumo, huduma za utoaji wa mizigo zitafanyika kwa ufanisi zaidi na kwa muda mfupi.


Hali hii itapunguza gharama za ucheleweshaji wa mizigo bandarini na kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa Tanzania katika soko la kikanda na kimataifa.


Faida kwa Serikali


Kwa Serikali, T-CAMS ni nyenzo muhimu ya kuongeza mapato na kuboresha usimamizi wa sekta.


Mfumo unarahisisha ufuatiliaji wa miamala, unapunguza mianya ya ukwepaji kodi na unatoa takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga sera na kuboresha huduma.


Aidha, uwazi wa miamala utaongeza uaminifu wa wawekezaji na taasisi za fedha katika mazingira ya biashara nchini.


Kuimarisha Ushindani wa Bandari za Tanzania

Bandari za Tanzania zinashindana na bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini. Mbali na miundombinu bora, ushindani huo unategemea pia kasi ya utoaji wa huduma na urahisi wa kufanya biashara.


Kwa kupunguza migogoro ya malipo, kuongeza uwazi na kuharakisha michakato ya biashara, T-CAMS itaongeza mvuto wa kutumia Bandari za Tanzania kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani.


Hitimisho


T-CAMS ni zaidi ya mfumo wa malipo. Ni mageuzi yanayolenga kujenga sekta ya uwakala wa forodha yenye uwazi, ushindani wa haki na ufanisi mkubwa.


Kwa mawakala wa forodha, mfumo huu ni kinga ya malipo na daraja la kukuza biashara zao. Kwa waagizaji wa mizigo, ni njia ya kupata huduma bora na za uhakika. Kwa Serikali, ni nyenzo ya kuongeza mapato, kuimarisha usimamizi na kukuza biashara.


Kadiri wadau watakavyoendelea kuunga mkono matumizi ya T-CAMS, ndivyo Tanzania itakavyozidi kujijengea sifa ya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati. Mfumo huu unawakilisha hatua muhimu kuelekea uchumi wa kisasa unaotumia teknolojia kuleta maendeleo jumuishi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Powered by Blogger.