WATU 16 WASWEKWA JELA KWA MAKOSA YA WIZI, UBAKAJI

 





 Tabora


JESHI la Polisi Mkoani Tabora limekamata jumla ya watuhumiwa 128 na kuwafikisha mahakamani kwa makosa mbalimbali ikiwemo wizi, ubakaji, mauaji, kujeruhi na kuharibu mali,16 kati yao wamehukumiwa kifungo.


Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Twaha Lulengelule amethibitisha kukamatwa watuhumiwa hao na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. 




Amefafanua kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika oparesheni maalumu iliyofanywa na askari polisi kuanzia Julai 1 mwaka huu hadi sasa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kwa lengo la kuimarisha amani na usalama.


Kamanda amebainisha kuwa miongoni mwa watuhumiwa 16 walioswekwa jela wapo waliohusika na makosa ya mauaji, ubakaji, wizi wa mali za watu, kujeruhi, kuharibu mali, kutishia kuua kwa silaha, shambulio la mwili na kutelekeza mtoto.


Ametaja aliyehukumiwa kwa kosa la kubaka kuwa ni Shaban Haruna Kilingo ambaye amefungwa miaka 30 jela huku Isack Majura Ryangera akihukumiwa kifungo cha mwaka 1 jela kwa kosa la kuua bila kukusudia.


Aidha katika oparesheni hiyo watuhumiwa 16 walikutwa na kilo 512 za bhangi na kete 1200 na wengine 50 wakiwa na lita 273 za pombe haramu ya moshi na mtambo wa kutengenezea na 14 walikutwa na nyara za serikali.


Kati ya hao 14 watuhumiwa 7 walikutwa na meno 2 ya tembo na vipande 9 vya meno hayo na watuhumiwa 7 wakakutwa na miguu 8 ya swala, vipande vya ngozi za wanayamapori na mazao ya misitu bila ya kibali.


Kamanda Lulengelule amedokeza kuwa pia walikamata watuhumiwa 14 wanaofanya shughuli za uganga bila kibali, watuhumiwa 11 wa wizi wa pikipiki na 5 wa wizi wa mifugo.


Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani ameeleza kuwa jumla ya madereva 18 walikamatwa na kufutiwa leseni za udereva kwa makosa ya mwendokasi, ulevi, kusababisha ajali na kuzidisha idadi ya abiria.


Kamanda amepongeza wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa kwa jeshi hilo na kuomba waendelea kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na wahalifu katika maeneo yao ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja.



Powered by Blogger.