BAKWATA TABORA WAPONGEZWA KUANZISHA MRADI WA KITEGA UCHUMI
Na Mwandishi wetu, Tabora
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoani Tabora limepongezwa kwa kuanzisha mradi wa kitega uchumi wa jengo la ghorofa tano utakaochochea maendeleo ya Baraza hilo, waumini na jamii kwa ujumla.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Waziri wa Ujenzi Alhaj Abdallah Hamis Ulega alipokuwa akitoa salamu za Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye Maulid ya Kumbukumbu ya Mazazi ya Mtume Muhammad S.A.W mjini hapa.
Ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais amewatakia kila la heri katika maulid hayo na ameomba waendelee kuombea amani na utulivu wa nchi ili vibaraka na wote wasioitakia mema nchi yetu wasipate nafasi.
‘Ndugu zangu nawaombeni tutumie hadhara hii kumwombea afya njema Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan na kuombea amani na utulivu wa nchi yetu, kwa kuwa mahali pasipo na amani na utulivu hakuna maendeleo’, ameeleza.
Waziri Ulega amebainisha wazi kuwa BAKWATA Tabora wana dhamira ya dhati kuinua uislamu na kujiletea maendeleo, ndiyo maana wameandaa maulid haya na kuwakutanisha waumini, viongozi na wageni kutoka maeneo mbalimbali.
‘Nakupongeza sana Shekhe wa Mkoa ndugu yangu Alhaj Ibrahim Mavumbi kwa maono yako mazuri ya kufanya maulid haya na kuanzisha mradi huu wa kimaendeleo, na mimi nitawachangia shilingi mil 10 ili kufanikisha mradi huu’, ameongeza.
Ametoa wito kwa BAKWATA Mkoa kuendelea kuhamasisha utoaji elimu ya dini kwa watoto wote wanaozaliwa katika familia za kiislamu ili kuwarithisha elimu hiyo kizazi hadi kizazi.
Shekhe wa Mkoa Alhaj Ibrahimu Mavumbi amemshukuru sana Mheshimiwa Waziri na wadau wote ambao wameendelea kuwaunga mkono ili kufanikisha mradi huo na kubainisha kuwa Oktoba 24, 2026 watafanya harambee kubwa ya kuchangia mradi huo.
Amedokeza kuwa mradi huo ni ubunifu waliofanya ili kuchochea maendeleo ya BAKWATA Mkoa, waumini na jamii kwa ujumla na kuongeza kuwa wananchi watapata ajira pia.



