KATIBU NEC ATAKA WENYE ULEMAVU KUCHANGAMKIA MIKOPO
Na mwandishi wetu, Tabora
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Rabia Hamid amewataka Vijana na Makundi mengine ya kijamii yenye ulemavu kuchangamkia mikopo inayotolewa na serikali ili kujikwamua kiuchumi.
Ametoa wito huo jana alipokuwa akiongea na wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Chama na Serikali, makundi ya kijamii na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukumbi wa Chuo cha Tabora Polytechnic.
Ameeleza kuwa fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazotolewa na serikali ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hazibagui mtu.
‘Nimetembea maeneo mbalimbali na kushuhudia vikundi vya vijana, akinamama na watu wenye ulemavu vikinufaika na mikopo nafuu isiyo na riba ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri pasipo ubaguzi wowote, hii ni fursa’, ameeleza.
Rabia amesisitiza kuwa watu wenye ulemavu wanaweza, hivyo wasikae nyumbani pasipo kufanya shughuli yoyote, mikopo inayotolewa na halmashauri ni fursa muhimu kwao, asiwepo wa kujinyanyapaa na kujiona kuwa hana uwezo.
Amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Madiwani na Maafisa Maendeleo ya Jamii kusaidia watu watu wenye ulemavu ili wanufaike na fursa za mikopo zilizopo, hii itachochea maisha yao kubadilika.
‘Serikali imetoa fursa nyingi zinazolenga kuinua maisha ya wananchi, naomba watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla tuzichangamkie, hakuna mtu anayeweza kubadilisha maisha yako, hatma ya maisha yako iko mikononi mwako’, ameongeza .
Katibu wa NEC amepongeza Ofisi ya Mkuu Mkoa wa Tabora kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Viongozi wa Chama hali ambayo imesaidia kuharakisha shughuli za maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Amefafanua kuwa serikali inatekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo ni muhimu sana kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali na Chama kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.
Akiwa Mkoani hapa Katibu wa NEC, anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Kamataifa Rabia Abdallah Hamid ametembelea miradi 3 ya vijana na akinamama na kujionea jinsi mikopo ya asilimia 10 ilivyowanufaisha kiuchumi.
Vikundi vya vijana ni Kazi Digital kilichowezeshwa mkopo wa sh mil 50 kwa ajili ya kutengeneza maudhui ya video ya taasisi mbalimbali na Umoja Group kilichowezeshwa mkopo wa sh mil 109 na kununua lori la kubeba madini ya ujenzi.
Kikundi cha akinamama ni FAMWA kilichowezeshwa mkopo na kuanzisha kiwanda cha kusaga na kukoboa mahindi na karanga na sasa wanasindika na kuuza ndani na nje ya Mkoa huo.



