WAKULIMA WA TUMBAKU TABORA WALILIA BEI NZURI

 





Na Mwandishi wetu, Tabora


WAKULIMA wa zao la tumbaku Mkoani Tabora wameeleza kusikitishwa na Makampuni yanayonunua zao hilo kujiamulia bei wanayotaka wenyewe wakati wa masoko jambo ambalo hupelekea mkulima kupata hasara kubwa.


Hayo yamebainishwa kwenye kikao cha siku moja cha Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku (WETCU) kilichofanyika jana katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Themi Hill mjini hapa.


Ismail Ramadhan , mkulima kutoka chama cha msingi Mwibiti, Wilayani Sikonge ameeleza kuwa katika msimu uliopita asilimia 80 ya tumbaku yao yote ilinunuliwa kwa bei ya dola 1.2 kwa kilo tofauti na bei elekezi ya dola 1.95.


‘Makampuni mengi yanatunyonya sana, haiwezekani bei elekezi ya soko kwa kilo ni dola 1.95 halafu mnunuzi aje kununua kwa bei anayotaka mwenyewe, hili haliingii akilini, huu ni wizi, tunaomba serikali itusaidie kuwadhibiti,’ ameeleza.


Gelard Kusaya, mkulima kutoka Wilaya ya Uyui, amelalamika kuwa bei ya tumbaku iko chini sana ukilinganisha na gharama halisi za kilimo hicho ikiwemo pembejeo, kama kampuni haiwezi kununua kwa bei elekezi ipigwe stop.




Ameongeza kuwa msimu uliopita wakulima wengi walipata hasara kutokana na bei ndogo ya wanunuzi hali iliyopelekea kushindwa kulipa madeni ya taasisi za fedha huku akiongeza kuwa bei ya pembejeo pia sio rafiki kwa mkulima.    


Shaban Mrisho mkulima kutoka Mibono Amcos ya Sikonge ameeleza kuwa kwa kuwa bei ya tumbaku haitabiriki, serikali iangalie uwezekanao wa kuwapunguzia bei ya pembejeo ili kuwapunguzia hasara wanayopata wakati wa masoko.


Maulid Chokala wa Mwanamkola Amcos ameomba serikali kupanga bei elekezi ya pembejeo mapema ili kumpunguzia mzigo mkulima, huku akiomba WETCU ipewe jukumu la kununua pembejeo na kusambazia wakulima kama ilivyokuwa zamani ili kuepusha usumbufu. 




Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella ameeleza kuwa mkutano huo ni muhimu sana kuelekea msimu mpya wa kilimo, hivyo akawahakikishia kuwa yote waliyosema atayafikisha kwa Mkuu wa Mkoa ili yafanyiwe kazi.


Aidha alishauri Chama Kikuu (WETCU) kuunda timu ya watu wachache kwa ajili ya kufuatilia malalamiko yao Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), timu hii itakuwa chini ya Mkuu wa Mkoa, hii itasaidia msimu mpya utakapoanza kusiwe na malalamiko yoyote.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Said Nkumba alieleza kuwa kilimo cha tumbaku kina faida kubwa kwa wakulima, hivyo akaomba serikali kusimamia kwa dhati bei ya zao hilo na kuangalia upya bei ya pembejeo ili isimuumize mkulima.



Powered by Blogger.