RC MALISA AAGIZA WATUMISHI KUTATUA KERO ZA WANANCHI

 





Na Mwandishi wetu, Tabora


KILA Mtumishi aliyepewa dhamana ya kutumikia wananchi ndani ya serikali hii Mkoani Tabora ametakiwa kuwa mstari wa mbele kusikiliza na kutatua kero zao na sio kusubiri hadi Viongozi wa ngazi za juu wafanye ziara katika eneo lao.


Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Benno Malisa alipokuwa akiongea na Viongozi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Wilaya na wengineo juzi.


Ameeleza kuwa kila mtumishi yupo kwa ajili ya wananchi hivyo anawajibu wa kusikiliza na kutatua kero yoyote inayomkabili mwananchi au kikundi cha wananchi inayohusiana na idara yake, huu ndio uwajibikaji wa kweli.


Amesisitiza kuwa viongozi au watumishi hawakuajiriwa ili wakae Ofisini tu kwenye kompyuta, bali kutembelea maeneo ya wananchi ili kujionea miradi inayotekelezwa, kusikiliza kero zao na kuangalia namna ya kuwasaidia.




RC ameagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi zote kuanzia Mitaa, Vijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa wananchi ili kupunguza malalamiko na kero zinaikabili jamii katika maeneo hayo.


 ‘Viongozi wa dini pia mna dhamana ya kusikiliza changamoto zinazowakabili waumini wenu na kuzitafutia ufumbuzi ili jamii iendelee kuishi kwa amani na utulivu na kumwabudu Mungu vizuri’, ameongeza.


Suala la kutatua kero za wananchi ni jukumu letu sote, tulibebe kwa pamoja na kila mmoja katika nafasi yake asikilize na kuzitatua, katika hili nahitaji sana ushirikiano wenu wa kutosha, ofisi yangu itakuwa wazi masaa 24’, amesema.




RC Malisa amebainisha kuwa wananchi wanataka maendeleo ndiyo maana serikali imeendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji miradi mbalimbali, hivyo akaelekeza isimamiwe ipasavyo na kama kuna kero itatuliwe.


Akiongea katika kikao hicho Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Ghullam-Hussein Dewj ameeleza kuwa RC aliyeondoka Paul Chacha alikuwa Kiongozi Karimu na RC aliyekuja ni Kiongozi Karimu pia, tutampa ushirikiano wa kutosha.



Powered by Blogger.