57,129 KUNUFAIKA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE TABORA

 



Na Mwandishi wetu, Tabora


KAYA 23,773 zenye wanufaika 57,129 Mkoani Tabora zinatarajiwa kunufaika na Huduma ya Bima ya Afya kwa Wote awamu ya pili baada ya kuzinduliwa kwa zoezi la uandikishaji wanufaika wapya.




Akitoa taarifa kwenye uzinduzi wa tukio hilo jana katika Uwanja wa TBC Mjini hapa, Meneja wa Kanda wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt Raphael Malaba ameeleza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu sana kwa ustawi wa jamii.


Amedokeza kuwa awamu ya kwanza walikadiria kufikia jumla ya kaya 15,870 zenye wakazi 70,145 lakini wakasajili wanufaika 27,046 kutoka kwenye kaya 9,981 ambao ni sawa na asilimia 63 ya walengwa wote katika Mkoa huo.


‘Awamu hii, tumelenga kusajili kaya 23,773 zenye wakazi 57,129 ili waweze kunufaika na matibabu mahali popote kwa kipindi cha mwaka mzima pasipo kusumbuliwa na mtu, kwa gharama ya sh 150,000 tu kwa wana familia 6’, alisema.


Dkt Malaba amesisitiza kuwa ili kufanikisha lengo hilo wamejipanga kutoa elimu ya kutosha na kuongeza hamasa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili kunufaika na huduma hiyo.   


Akizindua tukio hilo jana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Benno Malisa, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt Gerald Mongela amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mabilioni ya fedha ili kuboresha sekta ya afya nchini.




Aidha amempongeza Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa kwa kusimamia kwa dhati miradi yote inayotekelezwa na serikali katika sekta hiyo ikiwemo kuratibu uzinduzi wa huduma hiyo nchi nzima.


‘Rais anajali sana wananchi, ndio maana amepanua wigo wa upatikanaji huduma za afya kupitia Bima hii ya Afya kwa wote, ili makundi yote ya kijamii ikiwemo waendesha bodaboda, mamalishe na wananchi wote wanufaike’, ameeleza.


Dkt Mongella ametaja faida za Bima hiyo kuwa ni kupata matibabu ya uhakika na kwa wakati ambayo yatasaidia wananchi kupona haraka, kuzuia maambukizi kwa magonjwa yanayoambukizwa na kuimarisha uchumi wa wananchi.


Hivyo akatoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo wakati huu kabla ya dirisha kufungwa na kuwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha zoezi hilo linasimamiwa ipasavyo ili kusajili wananchi wengi zaidi.


Awali akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uzinduzi huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mohamed Nassoro Hamdan amempongeza Rais Samia kwa kutenga bajeti ili kutekelezwa huduma hiyo. 


Ameeleza kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza bayana kuwa Bima ya Afya itatolewa kwa wananchi wote hivyo akaomba watoa huduma kutoa elimu sahihi kwa jamii ili wananchi wengi wajisajili na kunufaika mwaka mzima.


Mwisho

Powered by Blogger.