IGUWASA YAONDOA KERO YA MAJI NKOKOTO
WANANCHI wa Kitongoji cha Nkokoto, Kata ya Igunga, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) kwa kuwafikishia huduma ya maji safi na salama, hatua iliyowaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti, wakazi wa Mtaa wa Setelite City katika Kitongoji hicho, Elizabeth Daudi, Hussein Mohammed, Catherine Samwel na Mwandu Jeremia, wamesema awali walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali iliyokuwa ikiwapotezea muda na kuwakwaza katika kutekeleza shughuli zao za maendeleo.
Wamesema upatikanaji wa huduma hiyo karibu na makazi yao umekuwa mkombozi kwa familia nyingi, hususan wanawake na watoto ambao awali walitumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kushughulikia majukumu mengine ya kila siku.
Aidha, wameipongeza IGUWASA, Wizara ya Maji pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa mradi huo, wakieleza kuwa huduma hiyo imeongeza matumaini ya kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa IGUWASA, Alexander Ntonge, amesema eneo hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo awali hayakuwa na makazi mengi ya watu, lakini kutokana na ongezeko la ujenzi wa nyumba na makazi ya wananchi, mamlaka hiyo imeona umuhimu wa kupanua mtandao wa maji ili kuwafikishia huduma wakazi hao.




