NEEMA YAWASHUKIA WATOTO WASIOJIWEZA MALOLO

 




Na Mwandishi wetu, Tabora


WATOTO wanaoishi katika mazingira magumu na wasiojiweza katika Kata ya Malolo, Halmashauri ya Manispaa Tabora wamepata neema baada ya kuchangiwa zaidi ya shilingi laki 5 katika harambee maalumu ili kuinua maisha yao.


Neema hiyo imeletwa na Mheshimiwa Diwani wa Kata hiyo Naomi Erasto Kasanga baada ya kuguswa na maisha ya watoto hao katika Kata yake hivyo kuamua kuandaa harambee ili kutunisha mfuko wa kuwasaidia.



Akiongea katika harambee hiyo, diwani Naomi ameeleza kufurahishwa na juhudi mbalimbali ambazo zimeendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha jamii inapata huduma zote za msingi katika maeneo yao.


‘Ndugu zangu serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mengi mazuri katika Kata yetu na Kata nyingine, na kuhakikisha watoto wetu wote wanapata huduma bora za afya na elimu’, amesema.


‘Tukio hili ni maalumu kwa ajili ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali yetu ili kuhakikisha watoto wote wa familia zenye


uwezo na zisizo na uwezo wanapata fursa sawa za kupata mahitaji ya msingi’, ameongeza.  


Diwani Naomi amefafanua kuwa kupitia harambee hiyo wameweza kukusanya zaidi ya shilingi laki 5 ambazo zitatumika kuhudumia watoto wote wanaoishi katika mazingira magumu katika vituo na maeneo mbalimbali ndani ya Kata hiyo.


Amesisitiza kuwa Kata hiyo ni miongoni mwa Kata zenye watoto wenye mahitaji mengi ya kibinadamu lakini hazijafikiwa vya kutosha, ndiyo maana ameamua kuandaa tukio hilo na kuita wadau mbalimbali ili wamuunge mkono kwa kuwachangia.


‘Ndugu viongozi, madiwani wenzangu, wanaCCM, wadau wa maendeleo, wageni waalikwa na wananchi wote nawashukuruni sana kwa moyo wenu wa upendo na kuniunga mkono katika hili, nawaomba tuendelee kusaidiana namna hii’, ameeleza.




Diwani Naomi amedokeza kuwa kiasi hicho kitasaidia watoto wote wasiojiweza waliopo katika Mitaa yote 7 ya Kata hiyo ambayo ni Kombomasai, Chang’ombe, Usenge, Mtakuja, Miyemba, UUzwxdxsxx,lamba Kanyenye na Urban Quarter.



Powered by Blogger.