AZIZ-KI NA YANGA HADI 2027

 Na Mwandishi Wetu Dar.


Mchezaji wa Klabu ya Yanga  raia wa Burkina-Faso Aziz-Ki amesaini mkataba wa miaka mitatu baada ya kufikia makubaliano na viongozi wa klabu hiyo kuhusiana na dau alilokuwa akihitaji mchezaji huyo.

Chanzo chetu cha Habari hii kutoka ndani ya Yanga kinaeleza, Aziz awali kupitia kwa meneja wake walitangaza kuhitaji dau kubwa la fedha ambalo uongozi ulishindwa kumudu.

"Hata hivyo Injinia Hersi (Rais wa Klabu hiyo) alikaa na viongozi wenzake, wakawasiliana na Mamake Aziz, wakaweka mambo sawa," kilieleza chanzo chetu hicho.

Ingawa kiasi cha pesa atakayolipwa mchezaji huyo anayewania kiatu cha mfungaji bora kwenye ligi Kuu ya NBC hakijajulikana, lakini taarifa zinaeleza kuwa huenda akawa ni mchezaji ghali zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Siku za hivi karibuni Rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said alikaririwa akisema anamtumza Aziz Ki kama mwanawe.

Yanga ambayo ni mabingwa mara 30 wa ligi Kuu ya Tanzania Bara iko katika harakati za kuwabakiza wachezaji wake wanaoelekea kumaliza mikataba yao baada ya kumalizika kwa msimu huku pia wakizisaka saini za wachezaji wengine, lengo likiwa  kuimarisha kikosi chao kinachotarajia kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.

Juhudi za kumpata Meneja Habari wa Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu mfululizo tangu ligi hiyo ianze kudhaminiwa na Benki ya Taifa ya Biashara(NBC PL) Ali Shaban Kamwe, hazikuzaa matunda baada ya simu yake muda mwingi kuelezwa kuwa inatumika.


Powered by Blogger.