SIMU JANJA ZIWASAIDIE KUPATA TAARIFA ZA MAENDELEO - WAZIRI DKT. GWAJIMA

 


Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ,Dkt. Dorothy Gwajima amewaasa wafanyabiashara ndogondogo kutumia simu janja walizonazo ziwasaidie kupata taarifa sahihi za fursa mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza na baadhi ya waendesha pikipiki (bodaboda) katika kituo kimoja cha eneo la Goba, wilaya ya Ubungo, Mei 21, 2024, ambao licha ya kuwa na simu janja walioonekana kutofahamu taarifa nyingi za fursa za maendeleo, Waziri Dkt. Gwajima aliweza kutoa elimu ya baadhi ya fursa za mikopo ya riba nafuu inayotolewa na baadhi ya benki nchini.

Amesema,  wakitumia vizuri mitandao ya kijamii kupitia simu zao watapata fursa nyingi kwa kujua mengi yanayotolewa na Serikali.

Waziri Dkt. Gwajima amepata wasaa wa kuwaelekeza namna ya kupata fursa hizo kwa kuhakikisha wanapata vitambulisho vya kielektroniki vinavyotolewa kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kote.

Amewasihi pia kutokatishwa tamaa na watendaji wasio na uadilifu badala yake wafuatilie kupitia simu za huduma kwa wateja za Wizara ya Maendeleo ya Jamii.

Kwa upande wao bodaboda hao wamesema wanatamani kupata fursa hizo lakini changamoto ni kukosa ushirikiano kwa baadhi ya watendaji pamoja na kutopata elimu sahihi ya nini wafanye.

Powered by Blogger.