TARURA YATENGA BIL 7 KUTENGENEZA KM 114 ZA BARABARA TABORA
Na Mwandishi wetu,TABORA
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani Tabora wanatarajia kutengeneza barabara zenye urefu wa km 114.05 kwa gharama ya sh bilioni 7.4 katika Wilaya ya Tabora Mjini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Hayo yamebainishwa jana na Meneja wa Wakala huo Wilaya ya Tabora, Mhandisi Subira Manyama alipokuwa akiwasilishwa rasimu ya mapendekezo ya bajeti ya TARURA kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Ametaja vipaumbele vya rasimu hiyo kuwa ni kukarabati barabara zote ambazo zimekuwa hazipitiki kwa kipindi kirefu ili ziweze kupitika wakati wote, kuzifanyia matengenezo barabara zote za mjini na vijijini ili ziwe imara zaidi.
Ameongeza kuwa watafanya matengenezo ya kawaida kwa sehemu korofi zote na ya muda maalumu kwa baadhi ya barabara ili kuwezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mazao yao kutoka vijijini kwenda kwenye masoko kwa mwaka mzima.
Mhandisi Manyama amefafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wanatarajia kutumia kiasi cha sh bil 7.4 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa km 114.05 na kujenga makalavati 11, boksi kalavati 10 na vivuko 11.
Aidha watajenga mifereji yenye urefu wa mita 3,300 kwa fedha za mfuko wa barabara, barabara ya kiwango cha zege km 0.1, changarawe km 3.98, makalavati mistari 19, vivuko 24 na mifereji mita 4,250 kwa fedha za tozo ya mafuta.
Meneja amedokeza kuwa pia watatengeneza km 11.5 za changarawe, boksi kalavati 1 na makalavati 5 kwa fedha za Mfuko wa Jimbo na matengenezo ya km 3.2 za barabara ya lami na mita 1200 za mifereji kwa fedha za Mfuko wa Barabara.
Akifafanua mpango wa matengenezo ya barabara hizo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund) amesema kuwa watafanya matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa km 98.8 kwa gharama ya sh milioni 348.9
Aidha sh milioni 230.5 zitatengeneza barabara korofi km 7.04 na sh milioni 162.6 matengenezo ya muda maalumu km 8.13 huku sh milioni 475 zikitumika kujenga makalavati, mifereji, vivuko na barabara za mlisho na mkusanyiko.


