ARTEMIS 2 YATUA SALAMA DUNIANI
Wanaanga wanne wa shirika la anga za juu la NASA waliokuwa kwenye misheni ya Artemis II wamerejea salama duniani baada ya kukamilisha safari ya kihistoria ya kuuzunguka Mwezi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50.
Chombo cha anga cha Orion kiliwabeba wanaanga hao na kutua baharini (splashdown) katika Bahari ya Pasifiki karibu na pwani ya California Aprili 10, 2026, baada ya safari ya takriban siku 10 angani.
Wanaanga hao—Reid Wiseman, Victor Glover, Christina Koch na Jeremy Hansen, walifanikiwa kuzunguka upande wa mbali wa Mwezi kabla ya kurejea duniani, wakivunja rekodi ya umbali mkubwa zaidi kuwahi kufikiwa na binadamu kutoka Dunia.
Katika hatua ya kurejea, chombo hicho kiliingia katika anga ya Dunia kwa kasi ya takribani maili 23,000 kwa saa, kikikumbana na joto kali na kukatika kwa mawasiliano kwa dakika kadhaa kutokana na msuguano wa hewa (plasma), hali ambayo ni ya kawaida katika misheni za aina hii.
Baada ya kutua, wanaanga walipokelewa na kikosi cha Jeshi la Wanamaji la Marekani na kufikishwa kwenye meli kwa uchunguzi wa afya kabla ya kurejeshwa katika kituo cha anga cha Johnson Space Center.
Misheni ya Artemis II ni hatua muhimu kuelekea malengo ya NASA ya kurejesha binadamu Mwezini katika miaka ijayo, ikiwa ni pamoja na mipango ya kutua rasmi juu ya uso wa Mwezi na baadaye safari za kwenda sayari ya Mirihi (Mars).
Safari hiyo pia imeweka historia kwa kuwa na mchanganyiko wa wanaanga wa jinsia na mataifa tofauti, ikiashiria ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa anga za juu.

