VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA RASILIMALI KULIINUA TAIFA KIUCHUMI
Mbunge wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza, Erick Shigongo, amesema Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa zilizopo kuendeleza Taifa na kuondokana na changamoto za umaskini, ujinga na maradhi.
Shigongo ameyasema hayo Aprili 11, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kando ya hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) lililoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, likiwa na lengo la kuwaunganisha vijana na kuwapatia taarifa muhimu zitakazowasaidia kujiletea maendeleo.
Amesema waasisi wa Taifa walikuwa na maono ya mbali, wakitambua uwepo wa rasilimali nyingi chini ya ardhi, lakini wakaamua kuzihifadhi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Waasisi na wazee wetu walijua kabisa kuwa chini ya ardhi kuna utajiri mkubwa kama uranium, almasi, dhahabu, gesi na Tanzanite. Baada ya uhuru wakaamini kuwa rasilimali hizi zitakuja kuwanufaisha watoto wao na vizazi vijavyo,” amesema Shigongo.
Aidha, amewataka vijana wa kizazi cha sasa kuchukua jukumu la kulisukuma mbele Taifa kwa kutumia rasilimali hizo kwa ufanisi na ubunifu, ili kupambana na maadui wakuu wa maendeleo waliotambuliwa tangu enzi za uhuru.
Ameongeza kuwa uzalendo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa, akiwahimiza vijana kupenda nchi yao na kuthubutu kama walivyofanya vijana wa mwaka 1961 waliopigania uhuru bila woga.
“Nimekuja kuzungumza na vijana kuhusu uzalendo, umuhimu wa kuipenda nchi yao na kuthamini fursa zilizopo. Vijana wa mwaka 1961 waliweka hofu pembeni na kusimama kidete kudai uhuru wa nchi yao, nasi tunapaswa kuiga moyo huo,” amesisitiza.
Shigongo amehitimisha kwa kuwataka vijana kutumia vyema urithi wa rasilimali waliouachiwa na wazee wao kwa ajili ya maendeleo ya sasa na vizazi vijavyo.


