REB YARIDHISHWA NA KASI YA MIRADI YA UMEME MWAMBAO WA ZIWA NYASA

 


Na Mwandishi Wetu, Ludewa

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeeleza kuridhishwa na kasi pamoja na ubora wa utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa, hususan katika wilaya za Ludewa na Makete.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara ya ukaguzi katika maeneo ya Nkanda na Lumbila, Mjumbe wa Bodi hiyo, Florian Haule, alipongeza juhudi zinazofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na mkandarasi, Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).



Haule alisema licha ya changamoto za kijiografia katika ukanda huo wa Bonde la Ufa, utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kasi ya kuridhisha, ambapo usimikaji wa nguzo umefikia hatua kubwa na kinachoendelea sasa ni uvutaji wa nyaya.


“Tumefurahishwa na hatua iliyofikiwa. Vifaa vyote muhimu vimeshafikishwa na hivi karibuni utaanza ufungaji wa transfoma,” alisema Haule.


Aliongeza kuwa mkandarasi ameihakikishia Bodi kukamilisha mradi huo ifikapo Julai 2026, jambo linalotoa matumaini kwa wananchi wanaosubiri huduma ya umeme katika maeneo hayo.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa REA, Mhandisi Yusuph Ismail, alisema hatua inayofuata ni usimikaji wa transfoma na ujenzi wa njia za umeme za msongo mdogo (LV) ili kuanza kuunganisha wateja wa awali.


Alibainisha kuwa katika kitongoji cha Nkanda, usimikaji wa nguzo kwa umbali wa takribani kilometa tisa umefikia hatua kubwa, huku matarajio yakiwa kuwasha umeme ifikapo Mei 25 mwaka huu.


“Tunawahimiza wananchi kufanya maandalizi ya ndani ya nyumba (wiring) ili waweze kuunganishiwa umeme mara moja huduma itakapoanza,” alisisitiza.


Aidha, Ismail alieleza kuwa upatikanaji wa umeme utachochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Nyasa, hususan katika sekta ya uvuvi kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za kuhifadhi samaki na kuongeza thamani ya mazao.


Huduma za kijamii zikiwemo shule, vituo vya afya, nyumba za ibada na ofisi za vijiji pia zinatarajiwa kunufaika na mradi huo, hali itakayoboreshwa utoaji wa huduma kwa wananchi.


Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya umeme ya SUMA JKT, Meja James Mhame, alisema zaidi ya asilimia 80 ya kazi ya awamu ya kwanza imekamilika.


“Tunatarajia kuanza uvutaji mkubwa wa nyaya pamoja na ufungaji wa transfoma ili kusambaza umeme kwa wananchi wa Nkanda na Lumbila,” alisema.

Kwa upande mwingine, Meneja Msimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Deogratius Nagu, alisema Serikali imetenga shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo katika Wilaya ya Ludewa.


Alifafanua kuwa changamoto za kijiografia, ikiwemo usafirishaji wa vifaa kwa njia ya maji na maeneo ya milimani, ndizo zilizopelekea jeshi kupewa jukumu la kutekeleza mradi huo.


“Maelekezo ya Bodi ni kuhakikisha wananchi wote walio tayari wanaunganishwa na umeme kabla mkandarasi hajaondoka, na tumejipanga kuyatekeleza kikamilifu,” alisema.

Miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wote wa vijijini, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni kama ukanda wa Ziwa Nyasa.


Powered by Blogger.