ZAIDI YA WATU 2,000 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA AFYA NJOMBE, OSHA YANG’ARA KITAIFA
Zaidi ya wafanyakazi na wananchi 2,000 kutoka Mkoa wa Njombe na maeneo mbalimbali nchini wamepatiwa huduma za afya kupitia Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Mji Mwema, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema mwitikio wa mwaka huu ulikuwa mkubwa zaidi huku taasisi na kampuni 150 zikishiriki ikilinganishwa na 70 za mwaka jana zilizofanyika mkoani Singida.
Mwenda amesema maadhimisho hayo pia yalivutia umati mkubwa wa wananchi waliotembelea mabanda mbalimbali na kujifunza masuala ya usalama na afya mahali pa kazi pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Ameeleza kuwa wananchi walipata huduma za afya kutoka kwa madaktari bingwa wa taasisi mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya.
“Maadhimisho haya yametia fora kwa i
dadi ya washiriki na huduma zilizotolewa, kwani zaidi ya wananchi 2,000 wamepatiwa huduma za afya na ushauri wa kisaikolojia,” amesema Mwenda.
Mbali na huduma za afya, OSHA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali walitoa vifaa kwa makundi tofauti ikiwemo waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na mama lishe, hatua inayolenga kuongeza usalama na kuboresha mazingira yao ya kazi.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amewahimiza wafanyakazi kutoa taarifa endapo sehemu zao za kazi hazina utambulisho wa OSHA, akisisitiza kuwa usajili wa waajiri ni muhimu kwa kuhakikisha usalama wa wafanyakazi.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu ameagiza OSHA, WCF na NSSF kuongeza kasi ya usajili wa waajiri na ukusanyaji wa madeni ndani ya siku 90, akibainisha kuwa bado waajiri wengi hawajazingatia sheria hali inayokwamisha ustawi wa sekta ya ajira nchini.



