TANTRADE YAUNGANISHA BIASHARA ZA TANZANIA - CONGO DRC
Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, hatua inayolenga kuimarisha biashara ya kikanda na kuongeza uwekezaji baina ya mataifa haya mawili.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, amesisitiza nafasi ya taasisi yake kama daraja la biashara la Tanzania, akiwakaribisha wafanyabiashara kutoka DRC kutumia fursa zilizopo nchini.
Ameeleza kuwa Tanzania imejipanga kurahisisha huduma za usafirishaji na kuimarisha biashara ya bidhaa za viwandani na vyakula ili kuongeza mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa kikanda.
Kwa upande wake, Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini (Bukavu), Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki, amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini DRC, akibainisha kuwa kuna nafasi nyingi za kibiashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Amengeza kuwa serikali ya DRC itaendelea kuhakikisha mazingira salama kwa wawekezaji, ili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukuza biashara ya kikanda.
Pamoja na hayo, Gavana ameelezea kuwa watajipanga kuhamasisha wafanyabiashara wa Kongo kutembelea na kishiriki fursa za Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba 2026.



