VODACOM TANZANIA YAWEKEZA ILI KUIMARISHA MUSTAKABALI WA M-PESA

 


Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM 

Kampuni ya Teknolojia na Mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc leo imetangaza kukamilika kwa maboresho makubwa ya huduma za M-Pesa kufuatia uwekezaji wa kimkakati wa dola za Marekani milioni 28 hatua inayoweka historia kama moja ya maboresho makubwa zaidi ya miundombinu ya kifedha (fintech) nchini.

Maboresho haya yanaihamisha huduma ya M-Pesa kutoka mfumo wa awali wa G2 kwenda kwenye mfumo wa kisasa wa teknolojia ya kifedha ulioboreshwa ili kuupa uwezo mkubwa zaidi, uthabiti na ubunifu, hatua inayoiwezesha kampuni hiyo kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za kifedha zilizo salama na zenye ufanisi hapa nchini.

Akizungumza kuhusu uwekezaji huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire alisema, “uwekezaji huu unalenga kuijengea M-Pesa misingi imara kwa ajili ya siku zijazo. Tunaimarisha huduma ya M-Pesa ili iendelee kuwa salama, ya kuaminika na yenye uwezo wa kusaidia maendeleo ya kiteknolojia. Wateja wetu wanastahili huduma inayo kua sambamba na mahitaji yao ya kasi zaidi, nguvu zaidi na uthabiti wa hali ya juu.”

Kwa upande wa wateja, maboresho haya yanaleta ufanisi zaidi kwa kupunguza changamoto za kukatika kwa huduma. Muundo wake wa kisasa unahakikisha kuwa matengenezo au maboresho ya mfumo yanafanyika ndani ya muda mfupi sana, kutoka masaa hadi dakika chache na hivyo kulinda mwendelezo wa miamala ya kila siku. Aidha, viwango vipya vya usalama vimeimarishwa zaidi kulinda taarifa na miamala ya wateja, na kuongeza imani katika huduma za fedha kwa njia ya simu.

Kwa mawakala, wafanyabiashara na washirika wa kibiashara, maboresho haya yanaleta uwezo mkubwa zaidi wa kushughulikia miamala, upatikanaji wa taarifa za kina pamoja na usimamizi wa huduma ulio wazi zaidi. Hii itasaidia kupanga biashara vizuri zaidi, kulinganisha hesabu za siku kwa urahisi na vilevile kuboresha huduma kwa wateja.

Maboresho haya pia yanawezesha huduma mpya kutambuliswa kwa urahisi na kwa haraka zaidi huku yakifungua fursa zaidi katika maeneo ya akiba, mikopo, malipo pamoja na huduma za biashara. Kadri huduma za kifedha kidijitali zinavyoendelea kukua nchini, M-Pesa sasa iko katika nafasi nzuri ya kupanuka kwa njia salama na endelevu.

Sehemu muhimu ya maboresho haya ni uwepo wa kipindi maalum cha siku 30 za huduma mahususi kwa Wateja (HyperCare), ambapo timu za kiufundi na huduma kwa wateja za Vodacom zitafanya kazi kwa karibu zikifuatilia na kushughulikia changamoto zozote zitakazojitokeza. Kipindi hiki kinalenga kuhakikisha watumiaji wote wanapata huduma bila usumbufu, huku maswali na changamoto zikitatuliwa kwa haraka na kwa weledi.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Vodacom Tanzania ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu na kuimarisha mageuzi ya kidijitali nchini. Kwa kuendelea kuimarisha M-Pesa, Vodacom inazidi kujenga nafasi yake kama mdau muhimu katika kukuza ujumuishwaji wa kifedha huku ikiendeleza fursa za uchumi jumuishi kwa Watanzania wote.

Powered by Blogger.