BEI YA PETROL YAZIDI KUPAA DAR ES SALAAM
Bei ya petroli katika Mkoa wa Dar es Salaam imepanda kwa Sh295 kwa lita na kufikia Sh4,115 mwezi Mei 2026 kutoka Sh3,820 mwezi uliopita, kufuatia EWURA kutangaza bei kikomo mpya za mafuta zitakazoanza kutumika kuanzia Mei 6, 2026 saa 6:01 usiku.
Katika bei hizo mpya zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), dizeli itauzwa kwa Sh4,248 kwa lita huku mafuta ya taa yakifikia Sh4,677 kwa lita katika jiji la Dar es Salaam.
EWURA imesema ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutokana na kuendelea kwa mvutano wa kisiasa na vita katika eneo la Mashariki ya Kati, hususan kati ya Marekani, Israel na Iran.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, unaopitisha karibu asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa duniani, kumeongeza gharama za usafirishaji na bima za meli za mafuta, hali iliyochochea ongezeko la bei za mafuta kimataifa.
Aidha, EWURA imesema Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka Mashariki ya Kati, hivyo mabadiliko ya bei katika eneo hilo yanaathiri moja kwa moja soko la ndani.
Pamoja na ongezeko hilo, Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya Sh259 kwa kila lita ya dizeli ili kupunguza makali ya bei kwa wananchi, hasa katika sekta za usafirishaji na shughuli za uzalishaji.
Kwa mujibu wa bei mpya, Tanga petroli itauzwa kwa Sh4,176 kwa lita na dizeli Sh4,309, wakati Mtwara petroli itakuwa Sh4,207 na dizeli Sh4,341 kwa lita.
EWURA imewataka wafanyabiashara kuuza mafuta kwa bei zisizozidi viwango vilivyotangazwa na wananchi kutoripoti vituo vitakavyokiuka maelekezo hayo



