IDADI YA WATUMIAJI WA BANGI IMEONGEZEKA DUNIANI NAKUFIKIA ASILIMIA 34




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi amesema idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya aina ya bangi duniani imeongezeka kwa asilimia 34 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita


Akiwasilisha taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Bungeni Jijini Dodoma leo, Mei 29, 2026 Prof. Kabudi amesema mwaka 2023 inakadiriwa Watu milioni 244 walitumia bangi duniani, sawa na asilimia 4.6 ya Watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64, huku kiwango cha matumizi kikiongezeka kwa asilimia 34 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita




Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Amerika Kaskazini ndiyo inayoongoza kwa kiwango cha matumizi ambapo takribani asilimia 20.2 ya Watu wa kundi hilo waliripotiwa kutumia bangi mwaka 2023. Pia imeelezwa kuwa bangi imeendelea kuwa chanzo kikuu cha Watu kuingia kwenye matibabu ya uraibu katika maeneo mbalimbali duniani.


Aidha, ripoti inaonyesha kuwa asilimia 42 ya watumiaji wa dawa za kulevya waliokuwa kwenye matibabu mwaka 2021 walitumia bangi, huku mwaka 2023 asilimia 41 ya Nchi zikiripoti bangi kuwa chanzo kikuu cha watu kuhitaji matibabu.


Barani Afrika, matumizi ya bangi yapo juu zaidi katika Kanda za Afrika ya Kusini, Magharibi na Kati, ambapo kiwango cha matumizi ya mwaka mmoja kimefikia takribani asilimia 10 ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64. Pia, asilimia 44 ya bangi iliyokamatwa duniani mwaka 2023 ilitoka Afrika.


Powered by Blogger.