MRADI WA EACOP UMETOA ZAIDI YA AJIRA 3,000 MKOANI SINGIDA-MHE.SALOME




Iramba, Singida


Zaidi ya ajira 3,000 zimetolewa mkoani Singida kupitia utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), huku wananchi wakinufaika pia kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kuuza vyakula, kukodisha vyombo vya usafiri na kutoa huduma nyingine zinazohitajika wakati wa utekelezaji wa mradi huo, hatua inayochangia kuongeza kipato kwa jamii zinazouzunguka mradi.



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema hayo leo Juni 13, 2026 wilayani Iramba mkoani Singida wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.


Amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kuwa Mradi wa EACOP hauwi tu mradi wa kukuza uchumi wa nchi bali unakuwa chachu ya kubadilisha maisha ya wananchi mmoja mmoja kupitia fursa za ajira na biashara.


Katika hatua nyingine, Mhe, Salome amesema kuwa ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote wilayani Iramba vitakuwa vimefikiwa na umeme ambapo kati ya vitongoji 393 vilivyopo tayari vitongoji 165 vina umeme na kwa sasa wakandarasi wanaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji 65.




Ameongeza kuwa Serikali  imetoa  shilingi milioni 285 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, mradi unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.


Vilevile amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 1.085 katika mwaka huu wa fedha unaoisha kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya umeme wilayani Iramba, ikiwemo kupunguza urefu wa laini za umeme na kuongeza transfoma ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.


Kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Salome  amesema Wilaya ya Iramba imepokea majiko banifu zaidi ya 1,000 na majiko ya gesi zaidi ya 2,000 ikiwa ni hatua za uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia, huku akitoa wito kwa wanaume kuwaunga mkono wanawake kwa kununua na kuhamasisha matumizi ya majiko hayo ili kuwawezesha kina mama kupata muda zaidi wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya familia.

Powered by Blogger.