RAIS DKT. MWINYI :SMZ KUENDELEA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono juhudi za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) katika utoaji wa elimu, kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 10 Juni 2026, alipokutana na ujumbe wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania uliofika Ikulu Zanzibar, ukiongozwa na Mkuu wa Chuo hicho na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza mchango wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kutoa fursa za elimu ya juu kwa wananchi wengi kupitia mfumo wa elimu huria na masafa, ambao umewezesha watu wa kada mbalimbali kuendelea na masomo bila kuathiri majukumu yao ya kila siku.
Rais Dkt.Mwinyi ameahidi kuendelea kushirikiana na Chuo hicho ili kuimarisha utoaji wa huduma za elimu Zanzibar na kuhakikisha wananchi wanapata fursa zaidi za kujiendeleza kielimu.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali italifanyia kazi ombi la kupatiwa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha uratibu wa elimu Unguja.
Vilevile, amepongeza uamuzi wa Chuo hicho wa kuanzisha kituo cha uratibu wa elimu Kisiwani Pemba na kuahidi kulifanyia kazi ombi la mchango wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa kazi kubwa inayofanywa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza kuwa elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda, amesema Chuo hicho kina mpango wa kujenga vituo vya kudumu vya uratibu Zanzibar ili kupunguza gharama za kukodi majengo na kukiwezesha kuwa na utambulisho wa kudumu kupitia miundombinu yake yenyewe.

