SERIKALI YAZIDI KUKEMEA MALIPO YASIYORASMI KWA WAJAWAZITO, YASISITIZA HUDUMA BURE


Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi amesema Serikali inaendelea kusisitiza utoaji wa huduma za afya bure kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, huku ikielekeza kusitishwa kwa malipo yasiyo rasmi yakiwemo gharama za vifaa kwa akinamama wanaokwenda kujifungua.


Akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Mjini, Mhe. Abdul Aziz Mohammed Abood, bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayotoa matibabu bure kwa makundi maalum ikiwemo wajawazito, watoto chini ya miaka mitano pamoja na wazee wasiokuwa na uwezo wenye umri wa zaidi ya miaka 60.


Amesema Serikali tayari imetangaza rasmi kuanza kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ambayo itahusisha makundi maalum ya wananchi wakiwemo wajawazito, watoto, watu wenye ulemavu na wazee wasiokuwa na uwezo.


Dkt. Samizi amesema gharama za matibabu kwa makundi hayo zitagharamiwa na Serikali, hatua itakayowezesha wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kupata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.


“Kukamilika kwa hatua hii kutasaidia wajawazito kupata huduma za afya kwa kugharamiwa na Serikali bila changamoto ya fedha,” amesema.


Aidha, Dkt. Samizi ametoa rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanafuata maelekezo ya Serikali kwa kutoa huduma kwa wajawazito pasipo kikwazo cha fedha.


"Serikali haitarajii kuona wajawazito wakitozwa malipo yasiyo rasmi wakati wa kupata huduma za uzazi, kwani huduma hizo zinapaswa kutolewa kwa mujibu wa sera na miongozo iliyowekwa", amefafanua Dkt. Samizi.


Utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na changamoto za upatikanaji wa huduma za uzazi.

Powered by Blogger.