SERIKALI YAENDELEA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA NCHINI




Serikali imeendelea kuvutia wawekezaji wakubwa katika sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini kufuatia uwepo wa kongani ya viwanda vya dawa Mloganzila, mazingira mazuri ya biashara pamoja na uhakika wa soko


Akizungumza leo Juni 01, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa, Bw. Emmanuel Tayari amesema Serikali imeendelea kupokea makampuni makubwa yenye nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa dawa, ikiwemo kampuni kutoka China iliyoorodheshwa katika soko la hisa la Shanghai Stock Exchange ambayo imeonesha nia thabiti ya kuwekeza katika uzalishaji wa dawa aina ya "generic drugs" kwa matumizi mbalimbali ya binadamu.


Amesema muamko wa uwekezaji katika sekta dawa umeendelea kuongezeka, huku baadhi ya wawekezaji wakubwa wakianza hatua za utekelezaji wa miradi yao katika eneo la viwanda la Mloganzila huku akidhihirisha kupitia utayari wa timu ya "Pharmaceutical Investment Acceleration Task Force" kwenye kuwasaidia wawekezaji wanaotaka kuingia katika sekta hiyo kwa kuwapa mwongozo na kuwezesha upatikanaji wa mazingira rafiki ya uwekezaji.

“Tanzania imeendelea kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji kutokana na uwepo wa soko kubwa la ndani pamoja na soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC. Kutokana na hali hii, tunawahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya dawa na vifaa tiba hapa nchini” amesema Bw. Tayari

Katika hatua nyingine, Bw. Tayari ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa msukumo na thamira ya dhati katika kuimarisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini. 

Aidha,ametoa Pongezi kwa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya sekta hiyo ambayo inalenga kuongeza upatikanaji wa dawa bora na huduma za afya kwa wananchi.

Powered by Blogger.