TAHADHARI YATOLEWA; VYAKULA VISIVYOONGEZWA VIRUTUBISHO VYAENDELEA KUCHANGIA WATOTO KUZALIWA NA MGONGO WAZI

 





Mwandishi wetu-Dar es salaam


Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kupambana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa virutubisho mwilini, bado matumizi ya vyakula visivyo na virutubisho yameendelea kuwa changamoto, hali inayochangia watoto kuzaliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo mgongo wazi na vichwa vikubwa.


Akizungumza Leo Juni 8,2026 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 40 wa Wadau wa Uongezaji Virutubisho Kwenye Vyakula, Mkurugenzi wa Huduma za Lishe kutoka TAMISEMI, Luitfrid Nnally, alisema Serikali imeendelea kutoa elimu na kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wazalishaji na wasindikaji wa vyakula wanaongeza virutubisho kwenye bidhaa zao kwa mujibu wa sheria.




Alisema uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula ni hatua muhimu katika kuzuia magonjwa yanayotokana na upungufu wa lishe, hususan kwa watoto na wanawake wajawazito.


“Tunawataka wote wanaojihusisha na biashara ya usindikaji wa vyakula kuhakikisha wanaongeza virutubisho kwenye bidhaa zao. Atakayebainika kukiuka sheria, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema Nnally.


Aidha, alieleza kuwa changamoto kubwa bado ipo kwa baadhi ya wakulima wanaozalisha mazao yao wenyewe, hususan mahindi, ambapo wengi hutumia unga unaotokana na mazao hayo bila kuongezwa virutubisho muhimu vinavyoweza kusaidia kuzuia magonjwa yanayohusiana na upungufu wa lishe.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA), Walter Miya, alisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wazazi na jamii kuhusu madhara ya upungufu wa virutubisho pamoja na namna ya kuwahudumia watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Powered by Blogger.