WANAFUNZI 246197 WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA UFUNDI WATAKIWA KURIPOTI KATIKA VITUO JULAI 4

 



DAR ES SALAAM — Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Riziki Shemdoe, amesema wanafunzi 246,197 waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya elimu ya ufundi mwaka 2026 wanapaswa kuripoti katika vituo walivyopangiwa kuanzia Julai 4 hadi Julai 31, 2026.


Akitoa taarifa kwa umma jijini Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema kati ya wanafunzi hao, 172,114 sawa na asilimia 69.9 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule za sekondari za Serikali, huku wanafunzi 74,083 sawa na asilimia 30.1 wakichaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya ufundi.


Amesema wanafunzi 3,144 wamepangiwa kujiunga na vyuo vinne vya elimu ya ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI).


Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa uchaguzi huo umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na mabadiliko ya shule au vyuo kutokana na uhaba wa nafasi.


Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ili kukidhi ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya kati nchini.



Powered by Blogger.